Askofu Bilionea
ASKOFU Bilionea na Nabii George David ‘Geordavie’ wa Kanisa la 
Geordavie Ministry ‘Ngurumo ya Upako’ lililoko jijini Arusha na Kawe, 
Dar hivi karibuni alifanya mkutano mkubwa na kutikisa nchi  kwa kuwa na 
magari ya kifahari na ndege aina ya helikopta ‘chopa’ iliyokuwa 
ikirandaranda juu ya anga kulinda usalama wake, Uwazi lina ushuhuda wa 
kutosha.
Katika mkutano huo uliofanyika Karatu mkoani Manyara, mwandishi wetu alishuhudia msafara wa Geordavie(Askofu Bilionea)
 ambaye hutoa huduma ya uponyaji kwa njia za miujiza, ukiwavutia watu 
wengi kwa kuwa ulikuwa na ulinzi mkali ambao haujawahi kutokea.
Mbali ya kuwa na chopa iliyokuwa ikiimarisha ulinzi ambayo ameinunua 
hivi karibuni, askofu huyo alikuwa na msururu wa magari yenye thamani 
kubwa yanayomfanya kutajwa kuwa tajiri kuliko maaskofu wengine wanatoa 
huduma katika makanisa ya kiroho Tanzania.
Alindwa na Jeshi la Polisi
Akiwa Karatu, mbali na ulinzi binafsi, Askofu Bilionea alikuwa 
akilindwa na askari wa jeshi la polisi, askari kanzu, Askari wa Kikosi 
cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wale wa usalama barabarani.
Mbali na askari hao wa serikali ambao wamekuwa wakimlinda kila 
anapofanya mikutano yake, pia Geordavie analindwa na askari wake binafsi
 hali iliyowafanya baadhi ya watu kuamini kuwa ulinzi wake ni kama ule 
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’.
Waumini wabaki na Mshangao.
“Sijawahi kumuona JK akilindwa na chopa lakini mtumishi wa Mungu 
Geordavie analindwa na ndege katika msafara wake! Hii ni mara yangu ya 
kwanza kuona,” alisema muumini mmoja ambaye hakupenda kutajwa gazetini.
Hata hivyo, baadhi ya watu walikuwa wakihoji utajiri wa askofu huyo 
kutokana na fedha nyingi anazozitumia anapofanya mikutano katika sehemu 
mbalimbali jijini Arusha.
“Tunajua kuwa ni tajiri, lakini anapata wapi fedha za kutumia hivi?” 
alihoji muumini aliyejitambulisha kwa jina moja la Julius ambaye naye 
alihudhuria mkutano wa askofu huyo anayetumia kaulimbiu ya Ngurumo ya 
Upako katika kutoa huduma yake.
Ugumu wa Kumwona
Pia, waumini wengine walilalamikia ugumu wanaoupata wanapotaka  
kumuona mtumishi huyo wa Mungu kutokana na ulinzi mkali anaopewa.
“Kila mtu alitamani kumuona mtumishi wa Mungu lakini haikuwezekana 
kutokana na ulinzi wake kuwa mkali, utajiri wake hakuna mfano, hata kule
 nyumbani kwake Arusha, anaishi kama Mfalme Daud,” alisema Fred Mushi.
Gazeti hili lilimsaka Askofu na Nabii Geordavie kwa lengo la kutaka 
kujua sababu ya kuwa na ulinzi mkali na kutumia magari ya kifahari 
ikiwemo chopa katika mikutano anayoifanya lakini simu yake iliita bila 
kupokelewa.
CREDIT: GPL






 5:05 AM
5:05 AM



 
 
 
 
 

0 comments:
Post a Comment