Thursday, February 27, 2014



Katika mfumo huo wa serikali mbili, waraka huo umependekeza Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais bila kujali kama Rais wa Jamhuri ya Muungano anatoka Bara au visiwani humo.
Waraka huo wa kurasa 22 unaoainisha mambo yenye masilahi kwa chama hicho, unawataka wajumbe wake kuutetea bungeni.Gazeti hili limefanikiwa kuona waraka huo, ambao pamoja na mambo mengine, umetoa mapendekezo katika ibara 42 za Rasimu ya Katiba ya Tume na kupangua hoja nyingi.
Katika miongoni mwa hoja hizo, chama hicho kimesisitiza muundo wa Muungano wa Serikali mbili lakini kikapendekeza kuwapo Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu waraka huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliukana akisema pamoja na msimamo wa chama hicho kuwa ni Serikali mbili, hakijafikia hatua ya kuwa na waraka.
Alisema vikao vya juu vya chama huwa havitoi waraka, bali msimamo na kwamba vyombo vingine vya chama ndivyo hutoa waraka, lakini hadi sasa havijafikia hatua hiyo.
Alisema kuwa alipoeleza maazimio ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alitaja msimamo wa chama hicho kuwa ni Serikali mbili zilizoboreshwa, lakini hakutaja maboresho hayo hata pale alipoulizwa na waandishi wa habari kwa sababu hayakuwa yamekamilika.
Hata hivyo, wajumbe watatu wa NEC kwa nyakati tofauti waliomba wasitajwe gazetini walisema mambo yaliyomo kwenye waraka huo ndiyo waliyokubaliana lakini hakuwa na uhakika kama ulishasambazwa.
Kwa mujibu wa waraka huo, chama hicho kinadaiwa kuainisha mambo kiliyopendekeza katika Rasimu ya Kwanza na jinsi yalivyoshughulikiwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Pia, kimeeleza mambo mengine mapya na kubainisha kasoro zake, ikiwamo utata katika mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.
Waraka huo pia unazungumzia sura mpya ya 17 katika Rasimu ya Katiba, ukisema inazungumzia mambo ya mpito kuelekea kupata Katiba Mpya, lakini gharama za utekelezaji wake hazitabiriki.
Sababu za Serikali mbili
Katika waraka huo, CCM kinadaiwa kueleza kuwa mapendekezo yake kuhusu muundo wa serikali mbili hayatokani na sera yake pekee, bali pia udhaifu uliojionyesha katika pendekezo la muundo wa Serikali tatu.
“Hivyo basi, CCM inapendekeza kwamba mfumo wa serikali mbili ufanyiwe marekebisho ambayo yatashughulikia changamoto zilizopo,” imesema sehemu ya waraka huo.
Wakati CCM kikitaka Muungano wa serikali mbili, Rasimu ya Pili ya Tume inapendekeza serikali tatu, sawa na zile zinazopigiwa chapuo na vyama vya Chadema na CUF.
Idadi ya Serikali katika muundo mpya wa Muungano, bado ni changamoto kutokana na hatua ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kugawanyika katika makundi yenye mitazamo tofauti.
Makamu wa Raisi
Katika mfumo huo wa serikali mbili, waraka huo umependekeza Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais bila kujali kama Rais wa Jamhuri ya Muungano anatoka Bara au visiwani humo.
“Rais wa Zanzibar katika Muungano, awe Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa na msaidizi wake kwa masuala ya Zanzibar na mmoja wa viongozi wakuu wa nchi,” imesema sehemu ya waraka huo na kuongeza:
“Hii itaongeza na kuweka wazi madaraka ya Rais wa Zanzibar ndani ya Serikali ya Muungano na nje ya nchi,” imesema sehemu ya waraka huo.
Muundo wa Bunge
Kuhusu Bunge, waraka huo unapendekeza kuwe na Baraza la Wawakilishi la Tanzania Bara kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Bara tu.
“Katika pendekezo hili, majimbo ya Jamhuri ya Muungano yaundwe upya na majimbo ya uchaguzi ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar yawe ndiyo hayohayo majimbo ya uchaguzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano,” ulisema waraka huo.
Waraka huo umependekeza Bunge la Muungano wakati linajadili mambo ya Muungano, wabunge wote washiriki majadiliano na inapofika kujadili mambo ya Tanzania Bara, washiriki wabunge wanaotoka Bara tu.
“Kama Spika anatoka sehemu moja ya Muungano, Naibu wake atatoka upande wa pili na wakati wa vikao vya masuala ya Bara Spika/Naibu Spika anayetoka Bara ndiye atakayeendesha kikao,” sehemu ya waraka huo inasema.
Waraka huo umependekeza masuala yasiyokuwa ya Muungano, kushughulikiwa na wabunge wa Tanzania Bara pekee.
Muundo wa mawaziri
Waraka huo umependekeza wajumbe wa Bunge la Muungano kuwa mawaziri wa wizara za mambo ya Muungano tu na wizara zisizo za Muungano ziongozwe na wabunge wanaotoka Tanzania Bara tu.
Pia umependekeza orodha ya mambo ya Muungano ambayo yatakuwa katika Katiba na mambo yasiyokuwa ya Muungano yaorodheshwe katika sheria itakayoainisha pia usimamizi, utekelezaji na gharama zake.
Mahakama
Kwa upande wa muundo wa Mahakama ya Juu, waraka umependekeza ndani ya mahakama hiyo kuwe na kitengo cha masuala ya Katiba tu.
Kuhusu misaada na mikopo nafuu kutoka kwa wahisani, umependekeza Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar, zijadili kwa kina kanuni ya mgawanyo wa fedha zinazotokana na vyanzo hivyo.
“Kuwekwe utaratibu wa kisheria wa kutenganisha misaada inayoelekezwa kwenye miradi ya Muungano na isiyokuwa ya Muungano,” ilisema sehemu ya waraka huo.
Usimamizi wa Muungano
Waraka huo umependekeza kuwapo kwa Tume ya Usimamizi na Uratibu wa mambo ya Muungano kikatiba na uendeshaji wake, kadhalika na mwenendo wa sasa wa vikao vya pamoja vinavyohusu kero za Muungano.
“Uratibu na usimamizi wa masuala ya Muungano uwekwe kisheria na Tume ipewe mamlaka ya kuzisimamia taasisi zote za Muungano katika makubaliano yatakayofikiwa na pande zote mbili,” unasema waraka huo.
Kuhusu Tume ya Pamoja ya Fedha
waraka huo unasema tume hiyo ambayo imetamkwa katika Katiba na kupitishwa na Sheria ya Bunge, imeshaundwa na mamlaka yake yanafahamika.
“Tunapendekeza Tume hii ipewe nguvu zaidi, iwekewe mfumo madhubuti wa kuiendesha na kuisimamia kwa karibu. Mapendekezo yanayotolewa na Tume yashughulikiwe na serikali zote mbili kwa haraka ili kama hakuna kikwazo, mapendekezo yake yatekelezwe bila kuchukua muda mrefu,” unasema.
Pia waraka huo umependekeza kufunguliwa kwa akaunti ya pamoja ya fedha zitokanazo na mapato ya vyanzo vya Muungano, kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwapo kwa utaratibu wa kisheria utakaoelekeza uendeshaji wa akaunti hiyo na kuweka mgawanyo wa mapato hayo kwa pande mbili za Muungano.
“Hii itasaidia sana kuwianisha uchumi wa pande hizo mbili. Sheria kuhusu utaratibu huo isimamiwe na Tume ya U husiano na Uratibu kama ilivyopendekezwa katika rasimu,” waraka huo unasema.
Chanzo Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Click here

Click here

Popular Posts