Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Rose Kamili amedai kupigwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati walipomkamata na kumshikilia kwa muda kwa tuhuma za kutoa rushwa.
Mbunge huyo kwa sasa amelazwa Hospitali ya Rufaa
ya Iringa akitibiwa majeraha yake na mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe amesema kwa sasa wanasubiri taarifa ya uchunguzi ili kuamua kama
ahamishiwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au KCMC.
“Wamenipiga, wamenidhalilisha vya kutosha,”
alisema mbunge huyo huku akitokwa na machozi. “Walipanua miguu yangu na
kunikanyaga sehemu za siri. Kama angekuwa mwanamume sijui angekuwa
katika hali gani?”
Alisema vitendo hivyo vilifanywa na walinzi wa
CCM, wanaojulikana kwa jina la Green Guard, ndani ya ofisi ya chama
hicho Mkoa wa Iringa na vilishuhudiwa na Mwenyekiti wa CCM wa Iringa,
Jesca Msambatavangu.
Muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana, Kamili
aliliambia Gazeti la Mwananchi kwamba wafuasi wa CCM walimteka wakati akitoa
maelekezo kwa mawakala wa Chadema waliokuwa wamepangwa kusimamia
uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kalenga.
Mbunge huyo alisema aliporwa Sh350,000, Pauni 500
za Uingereza, simu mbili; moja aina ya Nokia na nyingine Samsung, pamoja
na nakala 16 za daftari la wapigakura ambazo walikuwa wapewe mawakala
waliokuwa kwenye mkutano.
Wakati kukiwa na tuhuma utekaji uliofanywa na
wafuasi wa CCM, Msambatavangu alikiri jana kuwa chama hicho tawala
kilimshikilia kwa lengo la kumuhifadhi hadi polisi walipofika, lakini
akakanusha madai ya kuhusika kwa wafuasi wa CCM katika tukio hilo.
“Siyo kweli. Ni madai ya uongo na kama anadai hivyo tusubiri uchunguzi wa polisi ili ukweli ujulikane,” alisema Msambatavangu.
Kamanda wa Polisi wa Iringa, Ramadhani Mungi
alikiri kuwa polisi walimkuta Kamili kwenye ofisi za CCM za mkoa na
kwamba waliondoka naye baada ya kupewa taarifa na makada wa chama hicho
kwamba alikutwa akitoa fedha.
“Askari wetu waliokuwa kwenye msafara wa mgombea
wa CCM waliporudi, maana ilikuwa jioni, walimkuta huyo mtuhumiwa akiwa
kwenye ofisi za chama hicho ndipo walipompeleka kituoni,” alisema.
“Tuliambiwa amekutwa akitoa rushwa, lakini
alipofika kituoni naye akadai kwamba alitekwa, kupigwa na kudhalilishwa.
Sasa tumefungua majalada ya kuchunguza tuhuma zote mbili – suala la
rushwa na madai yake ya kutekwa.”
Kamanda Mungi alisema polisi hawafahamu mbunge huyo alikaa kwa muda gani kwenye ofisi za CCM kabla ya wao kumchukua.
Kuhusu ushiriki wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) katika suala hilo, Mungi alijibu: “Kazi ya polisi ni ya
polisi na ya Takukuru ni ya Takukuru, kama unataka kujua kuhusu wao
pengine ukawaulize.”
Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Iringa,
Emma Kuhanga aliwaongoza maofisa wake kwenda polisi kuitika wito wa
Kamanda Mungi aliyewaarifu kuwepo kwa mtu aliyekamatwa kwa rushwa.
Jana Kamanda Kuhanga alikiri kuitwa polisi lakini
akasema: “Ndiyo tulikwenda polisi, lakini tumeshindwa kushiriki kwenye
mchakato wa tuhuma hizo kwa sababu hatukupata maelezo yanayoeleweka.”
Alazwa hospitali
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine
Ishengoma jana alizuiwa na walinzi wa Chadema kumwona Kamili alipokwenda
kumjulia hali hospitalini.
Kuhusu tuhuma za rushwa, Msambatavangu alisema
wanakijiji waliizingira nyumba ambayo walihisi kwamba Kamili alikuwa
akigawa fedha na kuivamia kwa lengo la kuwakurupusha.
“Kwa kuwa baadhi ya vijana wetu walikuwa eneo
hilo, sisi tulichukua jukumu la kumpandisha haraka kwenye gari letu na
tulikimbia haraka maana tungemwacha pale wananchi wangemuumiza,” alisema
Msambatavangu ambaye alisema gari la Chadema lilifika eneo hilo na
kuzuia njia lakini wakafanikiwa kuondoka naye. ambaye alisema kundi la
wafuasi wa CCM wakiongozwa na Green Guard walivamia mkutano wa ndani wa
Chadema ambao ulikuwa ukiwapa mawakala maelekezo jinsi ya kusimamia
uchaguzi.
“Walikuwa wamemlenga mbunge yaani mimi,
walipotuvamia ilizuka taharuki na kunibeba na kunipandisha kwenye gari
kwa nguvu, ndani ya gari walikuwa wanaume tu na idadi yao ilikuwa ni
13,” alisema Kamili na kuongeza:
“Wakati gari linataka kuondoka, gari letu la M4C
lilizuia njia, na waliokuwa ndani ya gari waliambizana kwamba pita
porini hata tukipata ajali sawa tu…wakapita porini na walikimbia sana
hadi CCM mkoa ambako walianza kunitesa”.
Mbunge huyo alisema walipokuwa wakimpiga walikuwa
wakisema kwamba lazima wawakomeshe wabunge wa Chadema. “Waliniuliza
umekuja kufanya nini huku, kwani huku ni kwenu Manyara?...wakasema
lazima tuwakomeshe wabunge wa Chadema na hata kama ni kuua mmoja ili
mkome”.
0 comments:
Post a Comment