Wednesday, March 5, 2014

MFUNGWA aliyekuwa akitumikia kifungo cha miezi sita katika Gereza la Butundwe wilayani Geita amembaka mwanafunzi wa Shule ya Msingi Luhuha iliyoko Tarafa ya Butundwe na kumuumiza sehemu zake za siri, shingoni na kwenye jicho la kulia.
 Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa) alitendewa unyama huo na mfungwa aliyejulikana kwa jina la Godfrey Seleman (19) Februari 26, mwaka huu majira ya saa 9:00 alasiri wakati mwanafunzi huyo alipokuwa akichanja kuni na wanafunzi wenzake. 
Akieleza jinsi alivyofanyiwa unyama huo, mwanafunzi huyo alisema alipotoka shuleni akiwa na wasichana wenzake watano walikwenda kuchanja kuni ndipo walipomuona mfungwa huyo akiwa amevaa sare, lakini baadaye alitoweka ghafla na kurudi akiwa amejipaka masizi usoni, akiwa uchi kisha kuanza kumfukuza yeye huku wenzake wengine wakifanikiwa kukimbia huku wakipiga kelele. 
Alisema alizidiwa mbio na mfungwa huyo ambapo alimshika kisha kumkaba shingoni na kumwangusha chini na kuanza kumtendea unyama na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
“Baada ya kutendewa unyama huo nilitoka eneo hilo ambapo njiani nikutana na mama mmoja nikamwelezea mkasa ulionipata alinionea huruma ambapo alinipeleka ofisi ya kijiji ambako niliandikiwa barua kuwahi polisi, nikapelekwa hospitali ambako walinifanyia vipimo,” alisema binti huyo.
Aliendelea kusema kuwa mfungwa huyo alimpiga na kumuumiza katika jicho lake la kulia ambalo limevimba na kuwa bado anasikia maumivu makali jichoni na shingoni.Kamanda wa polisi mkoani hapa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo ameliita la kinyama lisilopaswa kutendwa na mtu mwenye akili timamu.
  Alisema mfungwa huyo mweye na namba 244/2013 alikuwa atoke kifungoni mwezi ujao, tayari ametiwa mbaroni na atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

0 comments:

Post a Comment

Click here

Click here

Popular Posts